slide

MFUMO MPYA TRA KURAHISISHA UTOAJI WA MIZIGO BANDARINI

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema matumizi ya mfumo mpya wa kuratibu mizigo inayotoka nje kuingia nchini utakuwa njia bora katika kuharakisha utoaji wa mizigo hiyo  mara inapoingia.
Hayo yalisemwa juzi na Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade wakati akimtembeza Rais Jakaya Kikwete katika idara mbalimbali za mamlaka hiyo katika maonyesho ya Sabasaba. 
              
“Tunatarajia mfumo huu utaongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi na kuharakisha clearance (utoaji wa mizigo kutoka nje), wataalamu wangu watakueleza jinsi unavyofanya kazi na faida zake kwa wadau mbalimbali,” alisema Bade.
Ofisa Msaidizi wa Huduma na Elimu kwa MlipaKodi, Chama Siriwa akitoa maelezo ya utendaji kazi wa mfumo huo ujulikanao kama TanCIS (Tanzania Customs Integrated System) alisema mpaka sasa tayari shughuli mbili zinaratibiwa chini ya mfumo huo.
“Tayari tunafanya cargo management (usimamizi wa mizigo) tangu Oktoba mwaka jana pamoja na clearance (kuondoa mizigo bandarini) tuliyoanza kuifanya Aprili Mosi, mwaka huu.
Ni mfumo uliounganishwa na mifumo mingine hivyo kurahisisha usalama na kazi nzima ya utoaji wa mizigo bandarini, alisema Siriwa.
 “Huu mfumo mpya utasaidia upataji wa taarifa kwa wakati miongoni mwa wadau. Hata mawakala wanautumia katika utoaji wa mizigo…waagizaji wa mizigo vilevile wataweza kuangalia mizigo yao imefikia hatua ipi na pia kujua imehifadhiwa sehemu gani,” alisema Siriwa na kubainisha kuwa ni mteja mwenye mzigo pekee atakayeruhusiwa kujua hilo kwa kutumia namba yake ya BL ili kuepusha wizi unaoweza kujitokeza.
Kwa hatua ya mwanzo, kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, mawakala wote wa Dar es Salaam wamesajiliwa kabla ya kuwahusisha na wale wa mikoani katika mfumo huo unaoruhusu wakala kukadiria kodi na mteja kuilipa kabla mzigo huo haujafika nchini.
“Kama taarifa za wakala zitalingana na manifest (nyaraka za usafirishaji) basi ataruhusiwa kutoa mzigo wake baada ya kulipa gharama zinazostahili tofauti na zamani ambapo tulikuwa tunasubiri mpaka shiper (msafirishaji) alete hiyo manifest,” alisema Siriwa.